32 Na mwenye kiburi atajikwaa, na kuanguka, wala hapana atakayemwinua; nami nitawasha moto katika miji yake, nao utawala wote wamzungukao pande zote.
33 BWANA wa majeshi asema hivi, Wana wa Israeli, na wana wa Yuda, wameonewa pamoja; na wote waliowachukua mateka wanawashika sana; wanakataa kuwaacha.
34 Mkombozi wao ni hodari; BWANA wa majeshi ndilo jina lake; yeye atawatetea kwa bidii, apate kuistarehesha nchi, na kuwasumbua wakaao katika Babeli.
35 Upanga u juu ya Wakaldayo, asema BWANA, na juu yao wakaao Babeli, na juu ya wakuu wake, na juu ya watu wake wenye hekima.
36 Upanga u juu ya hao wajisifuo, nao watapumbazika; upanga u juu ya mashujaa wake, nao watafadhaika.
37 Upanga u juu ya farasi zao, na juu ya magari yao ya vita; na juu ya watu wote waliochanganyika ndani yake, nao watakuwa kama wanawake; upanga u juu ya hazina zake, nazo zitaibwa.
38 Ukosefu wa mvua u juu ya maji yake, nayo yatakaushwa; maana ni nchi ya sanamu za kuchongwa, nao wameingiwa na wazimu kwa ajili ya sanamu.