23 na kwa wewe nitamvunja-vunja mchungaji na kundi lake; na kwa wewe nitamvunja-vunja mkulima na jozi yake ya ng’ombe; na kwa wewe nitawavunja-vunja maliwali na maakida.
24 Nami nitamlipa Babeli, na wote wakaao ndani ya Ukaldayo, mabaya yao yote, waliyoyatenda katika Sayuni mbele ya macho yenu, asema BWANA.
25 Tazama, mimi ni juu yako, Ee mlima uharibuo, asema BWANA; wewe uiharibuye dunia nzima; nami nitaunyosha mkono wangu juu yako, na kukufingirisha chini toka majabalini; nami nitakufanya kuwa mlima ulioteketezwa.
26 Wala hawatatwaa kwako jiwe moja liwe la pembeni, wala jiwe moja liwe msingi; bali wewe utakuwa ukiwa daima, asema BWANA.
27 Itwekeni bendera katika nchi, pigeni tarumbeta kati ya mataifa, yawekeni mataifa tayari juu yake; ziiteni juu yake falme za Ararati, na Mini, na Ashkenazi; agizeni jemadari juu yake; wapandisheni farasi, kama tunutu.
28 Wekeni mataifa tayari juu yake, wafalme wa Wamedi, na maliwali wake, na maakida wake, na nchi yote ya mamlaka yake.
29 Nayo nchi yatetemeka, nayo ina utungu; maana makusudi ya BWANA juu ya Babeli yasimama, kuifanya nchi ya Babeli ukiwa, isikaliwe na mtu.