12 Lakini enendeni sasa hata mahali pangu palipokuwapo katika Shilo, nilipolikalisha jina langu hapo kwanza, mkaone nilivyopatenda kwa sababu ya uovu wa watu wangu Israeli.
13 Na sasa, kwa sababu mmezifanya kazi hizi zote asema BWANA, nami nikasema nanyi, nikiamka mapema na kunena, lakini hamkusikia; nami nikawaita wala hamkuniitikia;
14 basi, nitaitenda nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, mnayoitumainia, na mahali hapa nilipowapa ninyi na baba zenu, kama nilivyopatenda Shilo.
15 Nami nitawatupa ninyi mbali na macho yangu, kama nilivyowatupa ndugu zenu wote, yaani, wazao wote wa Efraimu.
16 Basi, wewe usiwaombee watu hawa, wala usiwapazie sauti yako, wala kuwaombea dua, wala usinisihi kwa ajili yao; kwa maana sitakusikiliza.
17 Je! Huoni wanavyotenda katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu?
18 Watoto huokota kuni, na baba zao huwasha moto, na wanawake hukanda unga, ili kumfanyizia mikate malkia wa mbinguni, na kuwamiminia miungu mingine sadaka za kinywaji, wapate kunikasirisha mimi.