4 Nao wakakaribia mbele ya Eleazari, kuhani, na mbele ya Yoshua, mwana wa Nuni, na mbele ya mashehe, wakasema, BWANA alimwamuru Musa kutupa sisi urithi kati ya ndugu zetu; basi kwa kuiandama hiyo amri ya BWANA akawapa urithi kati ya ndugu za baba yao.
5 Kisha kura zilizomwangukia Manase zilikuwa ni sehemu kumi, mbali na nchi ya Gileadi na Bashani, iliyo ng’ambo ya Yordani;
6 kwa sababu hao binti za Manase walikuwa na urithi katika wanawe waume; na nchi ya Gileadi ilikuwa ni mali ya hao wana waume wa Manase waliosalia.
7 Mpaka wa Manase ulikuwa kutoka Asheri hata Mikmeta, ulioelekea Shekemu; tena mpaka ukaendelea upande wa kuume, hata kuwafikilia wenyeji wa Entapua.
8 Hiyo nchi ya Tapua ilikuwa ni mali ya Manase; lakini ule mji wa Tapua uliokuwa katika mpaka wa Manase ulikuwa ni mali ya wana wa Efraimu.
9 Tena mpaka ulitelemkia mpaka kijito cha Kana, upande wa kusini wa hicho kijito; miji hiyo ilikuwa ya Efraimu kati ya miji ya Manase; na mpaka wa Manase ulikuwa upande wa kaskazini wa hicho kijito, na matokeo yake yalikuwa baharini;
10 upande wa kusini ilikuwa ni mali ya Efraimu, na upande wa kaskazini ilikuwa ni mali ya Manase, na bahari ilikuwa mpaka wake; nao wakafikilia hata Asheri upande wa kaskazini, na kufikilia hata Isakari upande wa mashariki.