7 basi ninyi mtainuka mtoke hapo mwoteapo, na kuushika mji; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, atautia mikononi mwenu.
8 Kisha itakuwa, mtakapoushika mji, ndipo mtauteketeza mji kwa moto; sawasawa na hilo neno la BWANA; angalieni, nimewaagiza.
9 Basi Yoshua akawatuma; nao wakaenda hata hapo watakapootea, wakakaa kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa Ai; lakini Yoshua akalala usiku huo kati ya watu.
10 Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawakutanisha watu, kisha akatangulia kukwea kwenda Ai mbele ya hao watu, yeye na wazee wa Israeli.
11 Watu wote, hao wa vita, waliokuwa pamoja naye, wakaenda wakakaribia, na kufikilia mbele ya mji, wakatua upande wa kaskazini wa Ai; napo palikuwa na bonde kati ya yeye na Ai.
12 Kisha akatwaa watu kama elfu tano, akawaweka kuotea kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa huo mji.
13 Basi wakawaweka hao watu, jeshi zima lililokuwa upande wa kaskazini wa mji, na wale waliokuwa waotea upande wa magharibi wa mji; naye Yoshua akaenda usiku huo katikati ya hilo bonde.