6 Halafu Daudi aliweka kambi za kijeshi katika mji wa Shamu ya Damasko. Basi Waaramu wakawa watumishi wake, na wakawa wanalipa kodi. Mwenyezi-Mungu alimpa Daudi ushindi kokote alikokwenda.
7 Daudi alizichukua ngao za dhahabu walizobeba wanajeshi wa Hadadezeri, na kuzipeleka Yerusalemu.
8 Daudi alichukua pia shaba nyingi sana kutoka mji wa Tibhathi na mji wa Kuni; iliyokuwa miji ya Hadadezeri. Solomoni aliitumia shaba hiyo kutengenezea nguzo na vyombo vya shaba.
9 Wakati Tou, mfalme wa Hamathi aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri mfalme wa Soba,
10 alituma mwanawe Hadoramu kwa mfalme Daudi, kumpelekea salamu na pongezi kwa sababu alikuwa amepigana na Hadadezeri na kumshinda. Maana Hadadezeri alipigana na Tou mara nyingi. Hadoramu alimpelekea Daudi zawadi za vyombo vya fedha, dhahabu na shaba.
11 Zawadi hizo, mfalme Daudi aliziweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu pamoja na fedha na dhahabu aliyoiteka kutoka mataifa yote kutoka: Edomu, Moabu, Amoni, Filisti na Amaleki.
12 Abishai mwana wa Seruya, aliwaua Waedomu 18,000 katika Bonde la Chumvi.