1 Halafu Hana aliomba na kusema:“Namshangilia Mwenyezi-Mungu moyoni mwangu.Namtukuza Mwenyezi-Mungu aliye nguvu yangu.Nawacheka adui zangu;maana naufurahia ushindi wangu.
2 “Hakuna aliye mtakatifu kama Mwenyezi-Mungu;hakuna yeyote aliye kama yeye;hakuna aliye mwamba kama Mungu wetu.
3 Acheni kujisifu,acheni kusema ufidhuli.Maana ajuaye ni Mwenyezi-Mungu.Yeye huyapima matendo yote.
4 Pinde za wenye nguvu zimevunjika.Lakini wadhaifu wanaendelea kupata nguvu.
5 Wale ambao zamani walikuwa na chakula tele,sasa wanaajiriwa ili wapate chakula.Lakini waliokuwa na njaa,sasa hawana njaa tena.Mwanamke tasa amejifungua watoto saba.Lakini mama mwenye watoto wengi,sasa ameachwa bila mtoto.
6 Mwenyezi-Mungu huua na hufufua;yeye huwashusha chini kuzimunaye huwarudisha tena.
7 Mwenyezi-Mungu huwafanya baadhi wawe maskini,na baadhi wawe matajiri.Wengine huwashusha,na wengine huwakweza.