1 Kisha Daudi aliambiwa, “Sikiliza, Wafilisti wanaushambulia mji wa Keila na wanapora nafaka kwenye viwanja vya kupuria.”
2 Basi, Daudi akamwomba Mwenyezi-Mungu shauri, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti hawa?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Ndiyo, nenda ukawashambulie Wafilisti na kuuokoa mji wa Keila.”
3 Lakini watu wa Daudi wakamwambia, “Kama tukiwa hapahapa Yuda tunaogopa, itakuwaje basi, tukienda Keila na kuyashambulia majeshi ya Wafilisti?”
4 Daudi akamwomba tena shauri Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Inuka uende Keila kwani nitawatia Wafilisti mikononi mwako.”
5 Basi, Daudi akaenda Keila pamoja na watu wake, na huko akapigana na Wafilisti, akawaua Wafilisti wengi na kuteka nyara ng'ombe wengi. Hivyo Daudi aliwaokoa wakazi wa Keila.