10 Shauli akamwapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, akisema, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba hakuna adhabu yoyote itakayokupata kutokana na jambo hili.”
11 Yule mwanamke akamwuliza, “Je, nikuletee nani kutoka huko?” Shauli akajibu, “Niletee Samueli.”
12 Yule mwanamke alipomwona Samueli alilia kwa sauti kuu, akamwambia Shauli, “Kwa nini umenidanganya? Wewe ni Shauli!”
13 Mfalme Shauli akamwambia, “Usiogope! Unaona nini?” Yule mwanamke akamjibu, “Naona mungu akitokea ardhini.”
14 Shauli akamwambia mwanamke, “Ni mfano wa nani?” Yule mwanamke akamwambia, “Mwanamume mzee anapanda juu, naye amejizungushia joho.” Hapo, Shauli akatambua kwamba huyo ni Samueli. Shauli akainama hadi chini, na kusujudu.
15 Samueli akamwambia Shauli, “Kwa nini unanisumbua kwa kunileta juu?” Shauli akamjibu, “Mimi nina taabu kubwa! Wafilisti wanapigana vita dhidi yangu, na Mungu amenipa kisogo; hanijibu tena kwa njia ya manabii wala kwa ndoto. Ndio maana nimekuita unijulishe la kufanya.”
16 Samueli akasema, “Kwa nini unaniomba shauri ambapo Mwenyezi-Mungu amekupa kisogo na amekuwa adui yako?