5 Lazima mfanye vinyago vya majipu na vinyago vya panya wenu, vitu ambavyo vinaangamiza nchi yenu. Ni lazima mumpe heshima Mungu wa Israeli. Labda ataacha kuwaadhibu, nyinyi wenyewe, miungu yenu na nchi yenu.
6 Kwa nini mnakuwa wakaidi kama Wamisri na Farao? Je, Mungu alipowadhihaki Wamisri, hawakuwaacha Waisraeli waondoke, nao wakaondoka?
7 Basi, tayarisheni gari jipya na ng'ombe wawili wakamuliwao ambao bado hawajafungwa nira; wafungeni kwenye gari hilo lakini ndama wao wasiende pamoja nao, ila wabaki zizini.
8 Chukueni sanduku la Mwenyezi-Mungu na kuliweka katika gari hilo. Kando ya sanduku wekeni vile vinyago vya dhahabu ambavyo mnampelekea kama sadaka ya kuondoa hatia yenu. Kisha mliache liende litakakokwenda.
9 Bali angalieni, ikiwa gari hilo linakwenda moja kwa moja kuelekea nchi yake yaani kwenye mji wa Beth-shemeshi, basi, hapo tutajua kuwa aliyetuletea tauni hii ni Mungu wa Israeli. Lakini kama haliendi huko, basi, tutajua kuwa sio mkono wake uliotupiga, bali maafa haya yametupata kwa bahati mbaya.”
10 Walifanya kama walivyoambiwa; waliwachukua ng'ombe wawili wanaokamuliwa na kuwafunga kwenye gari, na ndama wao wakawafunga zizini.
11 Lile sanduku la Mwenyezi-Mungu wakalitia kwenye gari hilo pamoja na lile kasha lenye vinyago vya dhahabu vya panya na vile vya majipu.