2 Kishi alikuwa na mtoto wa kiume aliyeitwa Shauli. Shauli alikuwa kijana mzuri, na hakuna mtu katika Israeli aliyelingana na Shauli kwa uzuri. Shauli alikuwa mrefu zaidi kuliko mtu yeyote katika nchi ya Israeli; watu wote walimfikia mabegani.
3 Siku moja, punda wa Kishi, baba yake Shauli, walipotea. Hivyo, Kishi akamwambia Shauli, “Mchukue mmoja wa watumishi, uende kuwatafuta punda.”
4 Wakawatafuta kwenye nchi ya milima ya Efraimu na eneo la Shalisha, lakini hawakuwaona huko. Halafu wakafika Shalimu, na huko hawakuwaona. Wakawatafuta katika nchi ya Benyamini, hata hivyo hawakuwapata.
5 Walipofika kwenye nchi ya Sufu, Shauli alimwambia mtumishi wake, “Turudi nyumbani, la sivyo baba yangu ataacha kufikiria juu ya punda, na badala yake atakuwa na wasiwasi juu yetu.”
6 Yule mtumishi akamwambia, “Ngoja kidogo; katika mji huu kuna mtu wa Mungu ambaye anaheshimiwa sana; kila asemalo huwa kweli. Sasa tumwendee, labda anaweza kutuambia jinsi safari yetu itakavyokuwa.”
7 Shauli akamwuliza, “Lakini tukimwendea, tutampa nini? Tazama, mikate katika mifuko yetu imekwisha na hatuna chochote cha kumpa huyo mtu wa Mungu. Tuna nini?”
8 Yule mtumishi akamjibu Shauli, “Ona, mimi nina fedha robo shekeli. Nitampa huyo mtu wa Mungu ili atuambie juu ya safari yetu.”