5 Walipofika kwenye nchi ya Sufu, Shauli alimwambia mtumishi wake, “Turudi nyumbani, la sivyo baba yangu ataacha kufikiria juu ya punda, na badala yake atakuwa na wasiwasi juu yetu.”
6 Yule mtumishi akamwambia, “Ngoja kidogo; katika mji huu kuna mtu wa Mungu ambaye anaheshimiwa sana; kila asemalo huwa kweli. Sasa tumwendee, labda anaweza kutuambia jinsi safari yetu itakavyokuwa.”
7 Shauli akamwuliza, “Lakini tukimwendea, tutampa nini? Tazama, mikate katika mifuko yetu imekwisha na hatuna chochote cha kumpa huyo mtu wa Mungu. Tuna nini?”
8 Yule mtumishi akamjibu Shauli, “Ona, mimi nina fedha robo shekeli. Nitampa huyo mtu wa Mungu ili atuambie juu ya safari yetu.”
9 (Hapo awali katika Israeli kama mtu akitaka kumwomba Mungu shauri, alisema, “Haya, njoo, twende kwa mwonaji.” Kwani mtu anayeitwa nabii siku hizi hapo awali aliitwa mwonaji).
10 Shauli akamjibu, “Hilo ni jambo jema; haya, twende.” Hivyo, wakaenda kwenye mji alimokuwa anakaa yule mtu wa Mungu.
11 Walipokuwa wanapanda mlima kuelekea mjini, wakakutana na wasichana waliokuwa wakienda kuteka maji. Wakawauliza wasichana hao, “Je, mwonaji yuko mjini?”