1 Mara Athalia, mamake mfalme Ahazia, alipoona kuwa mwanawe ameuawa, alitoka, akaangamiza jamii yote ya kifalme.
2 Lakini Yehosheba binti ya mfalme Yoramu, dada yake Ahazia, alimchukua kwa siri Yoashi mwana wa Ahazia, kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Alimficha yeye pamoja na yaya wake katika chumba cha kulala. Hivyo walimficha ili Athalia asimwone na kumwua.
3 Yoashi alikaa naye kwa muda wa miaka sita akiwa amefichwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakati Athalia alipokuwa akitawala nchi.
4 Lakini katika mwaka wa saba Yehoyada alituma ujumbe na kuwakusanya makapteni wa Wakari na walinzi; akaamuru wamjie katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, naye akafanya nao mapatano na kuwaapisha humo katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Halafu akawaonesha Yoashi mwana wa mfalme Ahazia.