1 Katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi wa mwaka wa tisa wa utawala wake Sedekia, Nebukadneza mfalme wa Babuloni alifika na jeshi lake, akaushambulia mji wa Yerusalemu, akauzingira na kujenga ngome kuuzunguka.
2 Mji uliendelea kuzingirwa mpaka mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia.
3 Katika siku ya tisa ya mwezi wa nne njaa ilikuwa kali sana mjini hata hapakuwapo chakula chochote kwa ajili ya wakazi wake.
4 Basi, sehemu ya ukuta wa mji ilibomolewa, nao askari wote wakakimbia wakati wa usiku wakipitia katika bustani ya mfalme kwenye lango katikati ya kuta mbili, wakaenda upande wa Araba, ingawa Wababuloni walikuwa wameuzunguka mji.