4 “Mtu akimuua mwenzake bila kukusudia, naye hakuwa adui yake, anaweza kukimbilia mmojawapo wa miji hii, akayaokoa maisha yake.
5 Kwa mfano, mtu aendaye na mwenzake msituni kukata kuni naye wakati anakata mti, shoka likachomoka kutoka kwenye mpini wake, likamuua yule mwingine, mtu huyo anaweza kukimbilia kwenye mji mmojawapo, akayaokoa maisha yake.
6 Lakini kama umbali wa mji huo ni mkubwa mno, huyo mwenye kulipiza kisasi, kwa hasira kali anaweza kumfuatia, akamkamata na kumuua huyo aliyesababisha kifo, ingawaje hakupewa hukumu ya kifo na hao wahusika wawili hawakuwa maadui hapo awali!
7 Kwa hiyo mimi nawaamuru mtenge miji mitatu.
8 “Tena kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu ataipanua mipaka ya nchi yenu, kama alivyowaapia babu zenu, naye akawapatia nchi yote ambayo aliahidi kuwapatia hao babu zenu
9 ikiwa mtakuwa waangalifu kushika amri hizi zote ninazowaamuru hivi leo, mkampenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kufuata siku zote njia zake – basi, mtaongeza miji mingine mitatu zaidi ya hii mitatu,
10 ili mtu asiye na hatia asije akauawa katika nchi yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapatia kuwa yenu, na hivyo kuwasababisha kuwa na hatia ya mauaji.