1 “Zaidi ya hayo yote, utatengeneza hema takatifu kwa mapazia kumi ya kitani safi iliyosokotwa, na kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu. Mapazia hayo utayapamba kwa michoro ya viumbe wenye mabawa waliotariziwa.
2 Kila pazia litakuwa na urefu wa mita 12 na upana wa mita 2. Mapazia hayo yawe ya kipimo kimoja.
3 Utaunganisha mapazia matano yawe kipande kimoja na mapazia mengine matano yawe kipande cha pili.
4 Utashonea vitanzi vya buluu upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, hali kadhalika utashonea vitanzi mwishoni mwa pindo la nje la kipande kingine cha pazia.
5 Utatia vitanzi hamsini katika pazia moja na vitanzi vingine hamsini kwenye utepe wa pazia la pili; vitanzi vyote vielekeane.