26 Jambo hilo lilifanyika kote nchini Misri isipokuwa tu sehemu ya Gosheni walimokaa Waisraeli; humo haikuwako mvua ya mawe.
27 Basi, Farao akaagiza Mose na Aroni waitwe, akawaambia, “Safari hii nimetenda dhambi. Mwenyezi-Mungu ana haki; mimi na watu wangu tumekosa.
28 Mwombeni Mwenyezi-Mungu kwani ngurumo hii na mvua ya mawe vimezidi. Mimi nitawaacheni mwondoke na wala hamtakaa tena zaidi.”
29 Mose akamwambia, “Mara tu nitakapotoka nje ya mji nitainua mikono na kumwomba Mwenyezi-Mungu. Ngurumo itakoma na hakutakuwa na mvua ya mawe tena ili utambue kwamba dunia ni yake Mwenyezi-Mungu.
30 Lakini najua kwamba wewe na maofisa wako bado hammwogopi Mwenyezi-Mungu.”
31 (Kitani na mimea ya shayiri vyote vilikuwa vimeharibiwa, kwa sababu shayiri ilikuwa na masuke, na kitani ilikuwa imechanua maua.
32 Lakini ngano na jamii nyingine ya ngano havikuharibiwa kwa kuwa hiyo huchelewa kukomaa).