5 Basi, wana wa Israeli wakafika Misri wakiwa miongoni mwa wanunuzi wengine, kwani hata katika nchi ya Kanaani kulikuwa na njaa.
6 Wakati huo Yosefu alikuwa ndiye mkuu huko Misri. Yeye ndiye aliyehusika na kuwauzia wananchi nafaka. Basi, kaka zake wakaja na kumwinamia Yosefu kwa heshima.
7 Yosefu alipowaona kaka zake akawatambua, lakini akajifanya kana kwamba hawafahamu, akasema nao kwa ukali. Akawauliza, “Mmetoka wapi nyinyi?” Wakamjibu, “Tumetoka nchini Kanaani, tumekuja kununua chakula.”
8 Ingawa Yosefu aliwatambua kaka zake, wao hawakumtambua.
9 Akakumbuka ndoto zake za zamani juu ya kaka zake, akawaambia, “Nyinyi ni wapelelezi. Mmekuja kupeleleza udhaifu wa nchi yetu.”
10 Wao wakamjibu, “Sivyo, bwana wetu. Sisi watumishi wako tumekuja kununua chakula.
11 Sisi ni ndugu, wana wa baba mmoja. Sisi ni watu waaminifu, na wala si wapelelezi.”