1 Binadamu walipozidi kuongezeka duniani na kuzaa wasichana,
2 watoto wa kiume wa Mungu waliwaona hao wasichana wa watu kuwa ni wazuri, wakawachukua wale waliowapenda kuwa wake zao.
3 Hapo Mwenyezi-Mungu akasema, “Roho yangu haitakaa ndani ya binadamu milele, maana yeye ni wa kufa tu. Basi, hataishi zaidi ya miaka 120.”
4 Nyakati hizo na hata baadaye, kulikuwa na majitu duniani ambao walikuwa wazawa wa watoto wa kiume wa Mungu na wasichana wa watu. Hao ndio watu waliokuwa mashujaa na wenye sifa enzi hizo, nao waliitwa Wanefili.
5 Mwenyezi-Mungu alipoona wingi wa uovu wa binadamu duniani, na kwamba kila analokusudia binadamu moyoni mwake ni ovu daima,
6 Mwenyezi-Mungu alisikitika sana kwa kumuumba binadamu duniani. Mwenyezi-Mungu alihuzunika sana moyoni mwake,
7 hivyo akasema, “Nitamfuta kabisa duniani binadamu niliyemuumba; nitafutilia mbali pia wanyama wa porini, viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Ninasikitika kwamba niliwaumba duniani.”
8 Lakini Noa alipata fadhili mbele ya Mwenyezi-Mungu.
9 Ifuatayo ni habari juu ya Noa ambaye alikuwa ndiye mwadilifu pekee na ambaye hakuwa na lawama nyakati zake. Alikuwa mcha Mungu.
10 Noa alikuwa na watoto watatu wa kiume: Shemu, Hamu na Yafethi.
11 Mungu aliiona dunia kuwa imeharibika na kujaa ukatili.
12 Naam, Mungu aliiangalia dunia, akaona kuwa imeharibika kabisa, kwa maana kila mtu alifuata njia yake mbovu.
13 Mungu akamwambia Noa, “Nimeamua kuwaangamiza binadamu wote kwa sababu wameijaza dunia ukatili. Naam, nitawaangamiza kabisa pamoja na dunia!
14 Kwa hiyo, jitengenezee safina kwa mbao za mpingo. Gawa vyumba ndani yake na ipake lami ndani na nje.
15 Utaitengeneza hivi: Urefu wake mita 139, upana wake mita 25 na kimo chake mita 15.
16 Safina hiyo iwe ya ghorofa tatu na yenye mlango pembeni. Itengenezee paa, kisha acha nafasi ipatayo nusu mita kati ya paa na dari.
17 Nitaleta gharika ili kuangamiza viumbe vyote hai duniani. Kila kiumbe hai duniani kitakufa.
18 Lakini nitafanya agano nawe. Utaingia katika safina, wewe pamoja na mkeo, wanao na wake zao.
19 Nawe utaingiza katika safina jozi ya kila aina ya viumbe, wa kiume na wa kike, ili kuwahifadhi hai pamoja nawe.
20 “Utaingiza kila aina ya ndege wa angani, kila aina ya mnyama, kila aina ya kiumbe kitambaacho, wawiliwawili, ili kuwahifadhi hai.
21 Pia chukua aina zote za vyakula vinavyolika, uvihifadhi kwa ajili ya chakula chenu na viumbe hao.”
22 Noa akafanya yote kama Mungu alivyomwamuru.