1 Basi, Israeli akaanza safari yake pamoja na mali yake yote. Alipofika Beer-sheba, akamtolea tambiko Mungu wa Isaka, baba yake.
2 Mungu akaongea na Israeli katika maono usiku, akamwita, “Yakobo! Yakobo!” Yakobo akaitika, “Naam nasikiliza.”
3 Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu, Mungu wa baba yako. Usiogope kwenda Misri; utakapokuwa huko, nitakufanya uwe taifa kubwa.
4 Mimi mwenyewe nitakwenda pamoja nawe huko Misri na kukurudisha huku. Utakapofariki, mkono wa Yosefu ndio utakaoyafumba macho yako.”
5 Basi, Yakobo akaondoka Beer-sheba. Wanawe wakamchukua yeye, watoto wao wachanga pamoja na wake zao katika magari ambayo Farao alipeleka kumchukua.
6 Walichukua pia mifugo na mali yao yote waliyokuwa wamechuma katika nchi ya Kanaani, wakaenda Misri. Yakobo aliwachukua wazawa wake wote:
7 Wanawe, wajukuu wake wa kiume na wa kike, wote akawaleta Misri.
8 Wazawa wa Israeli ambao walikwenda Misri pamoja naye walikuwa Reubeni, mzaliwa wake wa kwanza,
9 pamoja na wana wa Reubeni: Henoki, Palu, Hesroni na Karmi.
10 Simeoni na wanawe: Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli, aliyezaliwa na mwanamke Mkanaani.
11 Lawi na wanawe: Gershoni, Kohathi na Merari.
12 Yuda na wanawe: Eri, Onani, Shela, Peresi na Zera. (Lakini Eri na Onani walifariki katika nchi ya Kanaani). Wana wa Peresi walikuwa Hesroni na Hamuli.
13 Isakari na wanawe: Tola, Puva, Yashubu na Shimroni.
14 Zebuluni na wanawe: Seredi, Eloni na Yaleeli.
15 Hao ndio wana ambao Lea alimzalia Yakobo kule Padan-aramu, pamoja na Dina binti yake. Jumla ya wanawe, binti zake na wajukuu wake walikuwa watu thelathini na watatu.
16 Gadi na wanawe: Sifioni, Hagi, Shuni, Esboni, Eri, Arodi na Areli.
17 Asheri na wanawe: Imna, Ishva, Ishvi, Beria na Sera, dada yao. Beria na wanawe: Heberi na Malkieli.
18 Hawa kumi na sita ni watoto na wajukuu wa Yakobo na Zilpa, mjakazi ambaye Labani alimpa Lea, binti yake.
19 Raheli alimzalia Yakobo wana wawili: Yosefu na Benyamini.
20 Huko Misri, Asenathi, binti Potifera, aliyekuwa kuhani wa mji wa Oni, alimzalia Yosefu wana wawili: Manase na Efraimu.
21 Wana wa Benyamini walikuwa Bela, Bekeri, Ashbeli, Gera, Naamani, Ehi, Roshi, Mupimu, Hupimu na Ardi.
22 Watu hao kumi na wanne ni watoto na wajukuu wa Yakobo na Raheli, mkewe.
23 Dani na Hushimu, mwanawe.
24 Naftali na wanawe: Yaseeli, Guni, Yeseri na Shilemu.
25 Hao saba ni watoto na wajukuu wa Yakobo na Bilha, mjakazi ambaye Labani alimpa binti yake Raheli.
26 Jumla ya wazawa wa Yakobo aliokwenda nao Misri, bila kuwahesabu wake za wanawe, ilikuwa watu sitini na sita.
27 Huko nchini Misri Yosefu alikuwa amepata wana wawili. Kwa hiyo watu wote wa jamaa ya Yakobo walioingia Misri walikuwa sabini.
28 Yakobo akamtanguliza Yuda kwa Yosefu kumwomba waonane huko Gosheni; nao wakafika katika eneo la Gosheni.
29 Yosefu akapanda gari lake la farasi, akaenda kumlaki Israeli, baba yake, huko Gosheni. Alipomfikia baba yake, alimkumbatia na kulia kwa kitambo kirefu.
30 Israeli akamwambia Yosefu, “Hata nikifa sasa si kitu kwa kuwa nimeuona uso wako na kujua kwamba wewe u hai!”
31 Yosefu akawaambia ndugu zake na jamaa yote ya baba yake, “Nakwenda kumwarifu Farao kwamba ndugu zangu na jamaa yote ya baba yangu waliokuwa katika nchi ya Kanaani wamekuja kwangu.
32 Nitamweleza kwamba nyinyi ni wachungaji kwani mmekuwa mkichunga mifugo, na kwamba mmewasili pamoja na mbuzi, kondoo, ng'ombe na mali yenu yote.
33 Basi, Farao akiwaita na kuwaulizeni, ‘Kazi yenu ni nini?’
34 Semeni: ‘Bwana, sisi watumishi wako, ni wafugaji wa mifugo tangu utoto wetu mpaka leo, kwani ndivyo walivyokuwa babu zetu’; semeni hivyo ili mruhusiwe kukaa katika eneo la Gosheni.” Yosefu alisema hivyo kwa sababu kwa Wamisri wachungaji wote wa kondoo ni chukizo.