1 Yakobo akawaita wanawe, akasema, “Kusanyikeni pamoja niwaambieni mambo yatakayowapata siku zijazo.
2 “Kusanyikeni msikie, enyi wana wa Yakobo,nisikilizeni mimi Israeli, baba yenu.
3 “Wewe Reubeni ni mzaliwa wangu wa kwanza,nguvu yangu na tunda la ujana wangu.Wewe wawapita ndugu zako kwa ukuu na nguvu.
4 “Wewe ni kama maji ya mafuriko.Lakini hutakuwa wa kwanza tena,maana ulipanda kitandani mwangu mimi baba yako,wewe ulikitia najisi;naam wewe ulikipanda!
5 “Simeoni na Lawi ni ndugu:Silaha zao wanatumia kufanya ukatili,
6 lakini mimi sitashiriki njama zao;ee roho yangu, usishiriki mikutano yao,maana, katika hasira yao, walimuua mtu,kwa utundu wao walikata mshipa wa ng'ombe.
7 “Nalaani hasira yao maana ni kali mno,na ghadhabu yao isiyo na huruma.Nitawatawanya katika nchi ya Yakobo,nitawasambaza katika nchi ya Israeli.
8 “Wewe Yuda, ndugu zako watakusifu.Adui zako utawakaba shingo;na ndugu zako watainama mbele yako.
9 “Wewe Yuda, mwanangu, ni kama mwanasimbaambaye amepata mawindo yake akapanda juu.Kama simba hujinyosha na kulala chini;simba mwenye nguvu, nani athubutuye kumwamsha?
10 “Fimbo ya kifalme haitatoka kwa Yuda,wala bakora ya utawala miguuni pake,mpaka atakapofika yule ambaye ni yake;ambaye mataifa yatamtii.
11 “Atafunga punda wake katika mzabibuna mwanapunda wake kwenye mzabibu bora.Hufua nguo zake katika divai,na mavazi yake katika divai nyekundu.
12 “Macho yake ni mekundu kwa divai,meno yake ni meupe kwa maziwa.
13 “Zebuluni ataishi sehemu za pwani,pwani yake itakuwa mahali pa kuegesha meli.Nchi yake itapakana na Sidoni.
14 “Isakari ni kama punda mwenye nguvu,ajilazaye kati ya mizigo yake.
15 “Aliona kuwa mahali pa kupumzikia ni pema,na kwamba nchi ni ya kupendeza,akauinamisha mgongo wake kubeba mzigo,akawa mtumwa kufanya kazi za shuruti.
16 “Dani atakuwa mwamuzi wa watu wake,kama mojawapo ya makabila ya Israeli.
17 “Atakuwa kama nyoka njiani,nyoka mwenye sumu kando ya njia,aumaye visigino vya farasi,naye mpandafarasi huanguka chali.
18 “Ee Mwenyezi-Mungu, nangojea uniokoe!
19 “Gadi atashambuliwa na wanyanganyi,lakini yeye atawafuata nyuma na kuwashambulia.
20 “Ardhi ya Asheri itatoa mavuno kwa wingi,naye atatoa chakula kimfaacho mfalme.
21 “Naftali ni kama paa aliye huru,azaaye watoto walio wazuri.
22 “Yosefu ni kama mti uzaao,mti uzaao kando ya chemchemi,matawi yake hutanda ukutani.
23 “Wapiga mishale walimshambulia vikali,wakamtupia mishale na kumsumbua sana.
24 “Lakini upinde wake bado imara,na mikono yake imepewa nguvu,kwa uwezo wa Mwenye Nguvu wa Yakobo,kwa jina la Mchungaji, Mwamba wa Israeli;
25 “kwa Mungu wa baba yako atakayekusaidia,kwa Mungu mwenye nguvu atakayekubariki;upate baraka za mvua toka juu mbinguni,baraka za maji ya vilindi vilivyo chini,baraka za uzazi wa akina mama na mifugo.
26 Baraka za baba yako zishinde baraka za milima ya milele,ziwe bora kuliko vilima vya kale.Baraka hizo na ziwe juu ya kichwa cha Yosefu,juu ya paji lake yeye aliyekuwa ametengwa na ndugu zake.
27 “Benyamini ni mbwamwitu mkali;asubuhi hula mawindo yake,na jioni hugawa nyara.”
28 Hayo ndiyo makabila kumi na mawili ya Israeli, na hayo ndiyo maneno aliyowaambia baba yao alipowabariki, kila mmoja wao kama alivyostahili.
29 Kisha Israeli akawaagiza wanawe hivi, “Mimi karibu nife na kujiunga na watu wangu. Nizikeni pamoja na wazee wangu katika pango lililoko shambani mwa Efroni Mhiti,
30 kule Makpela, mashariki ya Mamre, nchini Kanaani. Abrahamu alinunua pango na shamba hilo kwa Efroni, Mhiti, liwe lake la kuzikia.
31 Huko ndiko walikozikwa Abrahamu na mkewe Sara; huko ndiko walikozikwa Isaka na mkewe Rebeka; na huko ndiko nilikomzika Lea.
32 Shamba hilo na pango lake lilinunuliwa kwa Wahiti.”
33 Yakobo alipomaliza kuwausia wanawe, aliirudisha miguu yake kitandani, akatoa roho akajiunga na wazee wake.