1 Mwenyezi-Mungu akamwambia Noa, “Ingia ndani ya safina wewe pamoja na jamaa yako yote, kwa maana, kati ya watu wote wanaoishi nyakati hizi zako, nimekuona wewe peke yako kuwa mwadilifu mbele yangu.
2 Chukua pamoja nawe wanyama wote walio safi, dume na jike, saba saba; lakini wanyama walio najisi, chukua dume na jike, wawiliwawili.
3 Vilevile chukua ndege wa angani dume na jike, saba saba, ili kuzihifadhi hai aina zao duniani.
4 Baada ya siku saba, nitanyesha mvua nchini siku arubaini mchana na usiku, na kila kiumbe hai nilichokiumba duniani nitakiangamiza.”
5 Noa akafanya yote kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru.
6 Noa alikuwa na umri wa miaka 600 wakati gharika ilipotokea nchini.
7 Noa, mkewe, wanawe na wake zao wakaingia ndani ya safina ili kuiepa gharika.
8 Wanyama walio safi, wanyama walio najisi, ndege na viumbe vyote vitambaavyo,
9 wawiliwawili, dume na jike, wakaingia ndani ya safina pamoja na Noa kama Mungu alivyomwamuru.
10 Baada ya siku saba, maji ya gharika yakaanza kuifunika nchi.
11 Noa alipokuwa na umri wa miaka 600, mnamo siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili, siku hiyo chemchemi zote za vilindi vya nchi zikabubujika maji, na madirisha ya mbinguni yakafunguka.
12 Mvua ikanyesha nchini siku arubaini mchana na usiku.
13 Siku hiyohiyo mvua ilipoanza kunyesha, Noa, mkewe na wanawe, Shemu, Hamu na Yafethi, pamoja na wake zao, waliingia ndani ya safina.
14 Waliingia wao wenyewe pamoja na aina zote za wanyama wa porini, wanyama wafugwao, wanyama watambaao na ndege wa kila aina.
15 Waliingia ndani ya safina pamoja na Noa wiliwawili wa kila aina ya viumbe hai.
16 Kila aina yao waliingia, dume na jike, kama Mungu alivyomwamuru Noa. Kisha, Mwenyezi-Mungu akaufunga mlango wa safina nyuma yake Noa.
17 Gharika ilidumu nchini kwa muda wa siku arubaini. Maji yakaongezeka na kuiinua safina, ikaelea juu ya ardhi.
18 Maji yakaendelea kuongezeka zaidi nchini na safina ikaelea juu yake.
19 Maji hayo yakawa mengi sana juu ya nchi, yakaifunika milima yote mirefu katika nchi.
20 Yaliongezeka hata kuifunika milima kiasi cha mita saba na nusu.
21 Viumbe wote hai katika nchi wakafa. Ndege, wanyama wa kufugwa, wanyama wa porini, makundi ya viumbe wote katika nchi kavu na wanadamu wote;
22 naam, kila kiumbe hai katika nchi kavu kilikufa.
23 Mungu akaangamiza kila kiumbe kilichokuwa hai duniani: Binadamu, wanyama, viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Vyote viliangamizwa duniani. Noa tu ndiye aliyesalimika na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina.
24 Maji hayo yalidumu katika nchi siku 150.