1 Baada ya hayo, Yosefu alipewa habari kwamba baba yake ni mgonjwa. Hivyo, akawachukua wanawe wawili, Manase na Efraimu, akaenda nao kwa baba yake.
2 Yakobo alipofahamishwa kwamba mwanawe Yosefu amefika kumwona, akajitahidi kuinuka, akaketi kitandani.
3 Yakobo akamwambia Yosefu, “Mungu mwenye nguvu alinitokea nilipokuwa kule Luzu katika nchi ya Kanaani, akanibariki.
4 Aliniambia, ‘Tazama, nitakufanya uwe na wazawa na uongezeke; nitakufanya uwe babu wa jamii kubwa za watu. Ardhi hii nitawapa wazawa wako, waimiliki milele.’”
5 Yakobo akaendelea kusema, “Wanao wawili uliowapata hapa Misri kabla sijafika, ni wanangu; Efraimu na Manase watakuwa wangu kama walivyo Reubeni na Simeoni.
6 Lakini, watoto utakaopata baadaye watakuwa wako; kwa jina la ndugu zao wataitwa katika urithi wao.
7 Naamua hivyo kwa sababu ya mama yako, Raheli. Nilipokuwa narudi kutoka Padani yeye alifariki katika nchi ya Kanaani, tukiwa karibu kufika Efratha, akaniachia huzuni. Basi, nikamzika papo hapo, kando ya njia iendayo Efratha, yaani Bethlehemu.”
8 Israeli alipowaona wana wa Yosefu, akamwuliza, “Ni akina nani hawa?”
9 Yosefu akamjibu baba yake, “Hawa ni wanangu alionijalia Mungu nikiwa huku.” Israeli akasema, “Tafadhali, walete karibu nipate kuwabariki.”
10 Macho ya Israeli yalikuwa hayaoni vizuri kwa sababu ya uzee. Basi, Yosefu akawasogeza wanawe karibu na baba yake, naye akawabusu na kuwakumbatia.
11 Kisha Israeli akamwambia Yosefu, “Sikutazamia kuuona uso wako tena; lakini, kumbe, Mungu amenijalia hata kuwaona watoto wako!”
12 Hapo Yosefu akawaondoa wanawe kwenye magoti ya baba yake, kisha akainama kwa heshima.
13 Yosefu akawainua wanawe wawili, Efraimu katika mkono wake wa kulia, akimwelekeza kwenye mkono wa kushoto wa baba yake, na Manase katika mkono wake wa kushoto, akimwelekeza kwenye mkono wa kulia wa baba yake, akawasogeza kwa babu yao.
14 Lakini Israeli akaipishanisha mikono yake: Mkono wake wa kulia akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, ingawa alikuwa mdogo, na mkono wake wa kushoto akauweka juu ya kichwa cha Manase, aliyekuwa mzaliwa wa kwanza.
15 Kisha Israeli akambariki Yosefu, akisema,“Mungu ambaye babu zanguAbrahamu na Isaka walimtii maishani mwao,Mungu ambaye ameniongoza maishani mwangu hadi leo,
16 na malaika ambaye aliniokoa katika mabaya yote,na awabariki vijana hawa!Jina langu na majina ya wazee wangu, Abrahamu na Isaka,yadumishwe katika vijana hawa;nao waongezeke kwa wingi duniani.”
17 Yosefu alipoona kwamba baba yake ameuweka mkono wake wa kulia juu ya kichwa cha Efraimu hakupendezwa. Basi, akaushika mkono wa baba yake, akitaka kuuondoa juu ya kichwa cha Efraimu auweke juu ya kichwa cha Manase.
18 Akamwambia baba yake, “Sivyo, baba! Huyu hapa ndiye mzaliwa wa kwanza. Tafadhali, uweke mkono wako wa kulia juu ya kichwa chake.”
19 Lakini baba yake akakataa, akisema, “Najua, mwanangu, najua. Wana wa Manase pia watakuwa taifa kubwa na mashuhuri. Hata hivyo, ndugu yake mdogo atakuwa mkuu kuliko yeye, na wazawa wake watakuwa mataifa mengi.”
20 Basi, Israeli akawabariki siku hiyo, akisema,“Waisraeli watayatumia majina yenu kubarikia,watasema, ‘Mungu akutendee mema kama Efraimu na Manase!’”Ndivyo Israeli alivyomweka Efraimu mbele ya Manase.
21 Kisha Israeli akamwambia Yosefu, “Kama uonavyo, mimi niko karibu kufa. Hata hivyo, Mungu atakuwa pamoja nanyi, na kuwarudisheni katika nchi ya babu zenu.
22 Zaidi ya hayo, nimekupa wewe, wala si ndugu zako, eneo moja milimani, nililowanyanganya Waamori kwa upanga na upinde wangu.”