1 Abramu akarudi kutoka Misri, akaingia upande wa Negebu. Alikuwa na mkewe na mali yake yote pamoja na Loti.
2 Wakati huo, Abramu alikuwa ametajirika sana. Alikuwa na mifugo, fedha na dhahabu.
3 Akaendelea kusafiri toka eneo la Negebu hadi Betheli. Alifika mahali alipokuwa amepiga kambi ya hema hapo awali, kati ya Betheli na Ai,
4 ambapo alikuwa amejenga madhabahu. Hapo Abramu akamwomba Mwenyezi-Mungu kwa jina lake.
5 Kadhalika, Loti, ambaye alifuatana na Abramu, alikuwa na kondoo, mifugo na hema.
6 Idadi ya mifugo yao ilikuwa kubwa mno hata nchi ile haikuweza kuwatosha Abramu na Loti kuishi pamoja.
7 Basi, kukazuka ugomvi kati ya wachungaji wa Abramu na wachungaji wa Loti. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi ndio waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo.
8 Basi, Abramu akamwambia Loti, “Kusiwe na mafarakano kati yetu wala kati ya wachungaji wako na wachungaji wangu, kwa sababu sisi ni jamaa moja.
9 Tazama nchi hii yote mbele yako. Na tutengane. Ukienda kushoto, mimi nitakwenda kulia; ukienda kulia, mimi nitakwenda kushoto.”
10 Loti akatazama, akaliona bonde la mto Yordani, akaona kuwa lina maji ya kutosha kila mahali, kama bustani ya Mwenyezi-Mungu na kama nchi ya Misri upande wa Soari. (Hii ilikuwa kabla Mwenyezi-Mungu hajaiangamiza miji ya Sodoma na Gomora).
11 Kwa hiyo, Loti akajichagulia bonde lote la mto Yordani, akaelekea mashariki, na hivyo wakatengana.
12 Abramu akabaki nchini Kanaani na Loti akakaa kati ya miji iliyokuwa bondeni, akahamishia kambi yake Sodoma.
13 Watu wa Sodoma walikuwa waovu na watenda dhambi wakuu dhidi ya Mwenyezi-Mungu.
14 Baada ya Loti kujitenga na Abramu, Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Angalia toka hapo ulipo utazame pande zote: Kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi.
15 Nchi hii yote unayoiona nitakupa wewe na wazawa wako iwe yenu milele.
16 Wazawa wako nitawafanya wawe wengi wasiohesabika, kama vile mavumbi ya nchi yasivyoweza kuhesabika!
17 Basi, inuka uitembelee nchi hii katika mapana na marefu, kwani nitakupa wewe.”
18 Kwa hiyo, Abramu akangoa hema, akaenda kukaa karibu na mialoni ya Mamre kule Hebroni; huko akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu.