1 Mungu akambariki Noa na wanawe, akiwaambia, “Zaeni, muongezeke, mkaijaze nchi.
2 Wanyama wote, ndege wote wa angani, viumbe wote watambaao juu ya nchi na samaki wote wa baharini watakuwa na hofu na kuwaogopa nyinyi. Wote wamewekwa chini ya mamlaka yenu.
3 Wanyama wote hai watakuwa chakula chenu kama vile nilivyowapa mimea kuwa chakula chenu.
4 Lakini msile nyama yenye damu, kwani uhai uko katika damu.
5 Damu ya uhai wenu nitaidai; nitaidai kutoka kwa kila mnyama na binadamu. Atakayemuua binadamu mwenzake, nitamdai uhai wake.
6 Amwagaye damu ya binadamu,damu yake itamwagwa na binadamu;maana binadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu.
7 Nanyi zaeni, mkaongezeke;zaeni kwa wingi, mkaongezeke nchini.”
8 Kisha Mungu akamwambia Noa na wanawe,
9 “Ninaweka agano langu nanyi na wazawa wenu
10 na viumbe vyote hai: Ndege, wanyama wa kufugwa na wanyama wa porini, wote waliotoka katika safina pamoja nanyi.
11 Nathibitisha agano langu nanyi, kwamba, kamwe viumbe vyote hai havitaangamizwa kwa gharika, wala haitatokea tena gharika kuiharibu nchi.”
12 Tena Mungu akasema, “Hii ndiyo alama ya agano ninalofanya kati yangu nanyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi kwa vizazi vyote vijavyo.
13 Naweka upinde wangu mawinguni, nao utakuwa ishara ya agano kati yangu na dunia.
14 Kila nitakapoifunika dunia kwa mawingu, na huo upinde wa mvua utakapoonekana katika mawingu,
15 nitalikumbuka agano langu nanyi na viumbe vyote hai. Kamwe maji hayatageuka kuwa gharika ya kuviangamiza viumbe vyote hai.
16 Huo upinde utakapotokea mawinguni, nitauona na kulikumbuka agano hilo la milele kati yangu na viumbe vyote hai duniani.”
17 Mungu akamwambia Noa, “Hii ndiyo ishara ya agano ambalo nimefanya na viumbe vyote hai duniani.”
18 Watoto wa Noa waliotoka katika safina walikuwa Shemu, Hamu na Yafethi. Hamu alikuwa baba yake Kanaani.
19 Hao ndio watoto watatu wa Noa, na kutokana nao watu walienea duniani kote.
20 Noa alikuwa mkulima wa kwanza. Alilima shamba la mizabibu,
21 akanywa divai, akalewa, kisha akalala uchi hemani mwake.
22 Hamu, baba yake Kanaani, aliuona uchi wa baba yake, akatoka nje na kuwaambia ndugu zake wawili.
23 Lakini Shemu na Yafethi wakatwaa nguo, wakaitanda mabegani mwao, wakaenda kinyumenyume na kuufunika uchi wa baba yao. Waliangalia pembeni, wala hawakuuona uchi wa baba yao.
24 Noa alipolevuka na kujua alivyotendewa na mwanawe mdogo,
25 akasema,“Kanaani na alaaniwe!Atakuwa mtumwa wa watumwa kwa ndugu zake.”
26 Tena akasema,“Shemu na abarikiwe na Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu!Kanaani na awe mtumwa wake.
27 Mungu na amkuze Yafethi,aishi katika hema za Shemu;Kanaani na awe mtumwa wake.”
28 Baada ya gharika, Noa aliishi miaka 350,
29 kisha akafariki akiwa na umri wa miaka 950.