1 Kisha Mungu akamkumbuka Noa na wanyama wote wa porini na wa kufugwa waliokuwa pamoja naye ndani ya safina. Basi, Mungu akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakaanza kupungua.
2 Chemchemi za maji ya vilindi na madirisha ya mbinguni yakafungwa. Mvua ikazuiwa,
3 maji yakaendelea kupungua polepole katika nchi. Baada ya siku 150, maji yakawa yamepungua sana.
4 Mnamo siku ya kumi na saba ya mwezi wa saba, safina ikatua juu ya milima ya Ararati.
5 Maji yakaendelea kupungua polepole, na siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, vilele vya milima vikaonekana.