10 Sasa rudini nyumbani mkafanye sherehe, mle vinono na kunywa divai nzuri, lakini kumbukeni kuwapelekea wale ambao hawana cha kutosha; kwani leo ni siku takatifu kwa Bwana wetu. Msihuzunike kwa sababu furaha anayowajalia Mwenyezi-Mungu itawapeni nguvu.”
11 Hivyo, Walawi wakawatuliza watu wote, wakisema, “Tulieni kwani siku ya leo ni takatifu; msihuzunike.”
12 Watu wote wakarudi nyumbani kwao kula na kunywa; wakifurahi na kuwagawia wengine chakula kwa kuwa waliyaelewa yote waliyotangaziwa.
13 Kesho yake, wakuu wa koo pamoja na makuhani na Walawi wakakusanyika kwa Ezra mwandishi, ili kujifunza sheria.
14 Wakagundua kuwa, imeandikwa katika kitabu cha sheria kuwa Mwenyezi-Mungu alimwamuru Mose, kwamba watu wanapaswa kukaa vibandani wakati wa sikukuu ya mwezi wa saba.
15 Hivyo wakatangaza katika miji yao yote na huko Yerusalemu, wakisema, “Nendeni milimani, mkalete matawi ya mizeituni, mizeituni mwitu, mihadasi, mitende na miti mingineyo ili kujengea vibanda, kama ilivyoandikwa.”
16 Basi, watu wakaenda kuleta matawi, wakajijengea vibanda kila mtu kwenye dari na kwenye baraza ya nyumba yake, kwenye baraza za nyumba ya Mungu, kwenye uwanja wa Lango la Maji na uwanja wa Lango la Efraimu.