18 Waisraeli wakaenda Betheli kutaka shauri kwa Mungu, wapate kujua kabila ambalo litakwenda kwanza kupigana na watu wa kabila la Benyamini. Mwenyezi-Mungu alitaja kabila la Yuda liende kwanza.
19 Basi, Waisraeli wakaenda asubuhi, wakapiga kambi yao karibu na mji wa Gibea.
20 Waisraeli wakatoka kupigana na watu wa kabila la Benyamini karibu na Gibea.
21 Watu wa kabila la Benyamini wakatoka nje ya mji wa Gibea wakapigana na Waisraeli, wakawaangusha chini siku hiyo, watu wa Israeli 22,000.
22 Lakini Waisraeli wakajipa moyo, wakajipanga tena kwa vita mahali pale walipojipanga kwa mara ya kwanza.
23 Basi Waisraeli wakaenda juu, wakamlilia Mwenyezi-Mungu mpaka jioni. Kisha wakaomba shauri kwa Mwenyezi-Mungu: “Je, twende tena kupigana na ndugu zetu, wa kabila la Benyamini?” Mwenyezi-Mungu akawajibu, “Nendeni mkapigane nao.”
24 Hivyo siku ya pili Waisraeli wakakaribia kupigana na watu wa kabila la Benyamini.