26 Watu wote wa jeshi la Waisraeli wakaenda Betheli. Walikaa huko mbele ya Mwenyezi-Mungu wakiomboleza na kufunga mpaka jioni. Wakamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani.
27 Waisraeli wakamwomba Mwenyezi-Mungu awape shauri. Wakati huo sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilikuwa huko Betheli.
28 Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Aroni alikuwa na wajibu wa kuhudumu mbele yake. Waisraeli wakamwuliza Mwenyezi-Mungu, “Je, twende tena kupigana na ndugu zetu, watu wa kabila la Benyamini?” Mwenyezi-Mungu akawaambia, “Nendeni. Kesho nitawatia mikononi mwenu.”
29 Hivyo, Waisraeli wakaweka watu mafichoni kuuzunguka mji wa Gibea.
30 Waisraeli wakaenda kupigana na watu wa kabila la Benyamini katika siku ya tatu. Wakajipanga dhidi ya mji wa Gibea kama walivyofanya nyakati za hapo awali.
31 Kisha watu wa kabila la Benyamini walipotoka mjini kuanza kupigana na Waisraeli, walivutwa kutoka nje ya mji. Ilitokea tena kama walivyofanya nyakati za hapo awali wakawaua baadhi ya watu wa Israeli kwenye njia kuu zielekeazo miji ya Betheli na Gibea, mpaka mbugani. Waliua Waisraeli wapatao thelathini.
32 Watu wa Benyamini wakafikiri, “Tumewapiga kama nyakati zilizopita.” Lakini Waisraeli wakasema, “Sisi tukimbie ili tuwavute mbali na mji hadi kwenye njia kuu.”