23 Kisha, Ehudi akatoka nje barazani baada ya kuifunga milango ya chumba hicho kwa ufunguo.
24 Ehudi alipoondoka, watumishi wa mfalme wakarudi. Walipoona milango yote ya chumba imefungwa, walifikiri amekwenda kujisaidia chooni humo ndani ya nyumba.
25 Wakangojea mpaka wakaanza kuwa na wasiwasi. Walipoona hafungui, wakachukua ufunguo na kufungua mlango. Wakamwona mfalme wao sakafuni, naye amekufa.
26 Walipokuwa wanangoja, Ehudi alitoroka akipitia kwenye sanamu za mawe, akaenda Seira.
27 Alipofika huko alipiga tarumbeta katika nchi ya milima ya Efraimu, nao Waisraeli wakateremka pamoja naye kutoka huko milimani naye akawatangulia.
28 Akawaambia, “Mnifuate, maana Mwenyezi-Mungu amewatia adui zenu Wamoabu mikononi mwenu.” Wakamfuata mpaka kivuko cha Yordani na kukiteka toka mikononi mwa Wamoabu, wakazuia mtu yeyote kupita.
29 Siku hiyo, wakawaua Wamoabu wapatao 10,000; watu wote wenye afya na nguvu, wala hakuna hata mmoja aliyenusurika.