14 Mwenyezi-Mungu akamgeukia, akamwambia, “Nenda kwa uwezo ulio nao, ukaikomboe Israeli kutoka Wamidiani. Ni mimi ninayekutuma.”
15 Gideoni akamjibu, “Tafadhali Bwana, nitawezaje kuikomboa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu zaidi katika kabila la Manase, na mimi mwenyewe ni mdogo kabisa katika jamaa yetu!”
16 Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nitakuwa pamoja nawe; nawe utawaangamiza Wamidiani kana kwamba wangekuwa mtu mmoja.”
17 Gideoni akamwambia, “Basi, ikiwa nimepata fadhili kwako, nioneshe ishara ili nijue kuwa ni wewe kweli uliyezungumza nami.
18 Nakuomba usiondoke hapa mpaka nitakaporudi na kukuletea zawadi yangu na kuiweka mbele yako.”Naye akamjibu, “Nitakaa hapa mpaka utakaporudi.”
19 Gideoni akaenda nyumbani mwake, akatayarisha mwanambuzi na mikate isiyotiwa chachu kutoka debe la unga; akatia nyama ndani ya kikapu na mchuzi ndani ya chungu, kisha akampelekea chini ya mwaloni, akampa.
20 Malaika wa Mungu akamwambia, “Chukua nyama na mikate isiyotiwa chachu uviweke juu ya mwamba huu. Halafu tia mchuzi juu ya mikate na nyama.” Naye akafanya hivyo.