27 Basi, Gideoni akachukua watumishi wake kumi, akafanya kama alivyoagizwa na Mwenyezi-Mungu. Lakini kwa kuwa aliiogopa jamaa yake na watu wa mjini, badala ya kufanya hayo mchana, alifanya wakati wa usiku.
28 Wakazi wa mji walipoamka asubuhi na mapema waliona madhabahu ya Baali na sanamu ya Ashera iliyokuwa karibu nayo vimeharibiwa. Yule fahali wa pili alikuwa ameteketezwa juu ya madhabahu iliyokuwa imejengwa mahali hapo.
29 Wakaulizana, “Nani amefanya jambo hili?” Walipofanya uchunguzi wakagundua kwamba Gideoni mwana wa Yoashi ndiye aliyekuwa amefanya hayo.
30 Wakazi wa mji wakamjia Yoashi, wakamwambia, “Mtoe mwanao tumuue, maana ameharibu madhabahu ya Baali na kuivunja sanamu ya Ashera iliyokuwa karibu nayo.”
31 Yoashi akawaambia wale wote waliomkabili, “Je, mnamtetea Baali? Je, mtamwokoa? Yeyote atakayemtetea atauawa kabla ya mapambazuko. Kama Baali ni mungu, basi, na ajitetee mwenyewe maana madhabahu yake imebomolewa.”
32 Siku hiyo wakamwita Gideoni “Yerubaali” maana yake, “Baali na ajitetee mbele yake”, maana aliibomoa madhabahu ya Baali.
33 Wamidiani, Waamaleki na watu wote wanaokaa kando ya mto Yordani wakapiga kambi zao katika bonde la Yezreeli.