15 Kisha, kuhani atachukua kiasi cha ile theluthi moja ya mafuta na kuyatia katika kiganja cha mkono wake wa kushoto.
16 Atachovya kidole cha mkono wake wa kulia katika mafuta hayo na kumnyunyizia huyo mtu anayetakaswa mara saba mbele ya Mwenyezi-Mungu.
17 Kiasi cha mafuta yanayobaki katika kiganja chake atampaka huyo mtu anayetakaswa katika ncha ya sikio lake la kulia na kidole gumba cha mkono wake wa kulia na kidole gumba cha mguu wake wa kulia, mahali palepale alipompaka damu ya sadaka ya kuondoa hatia.
18 Yale mafuta yaliyobaki atampaka huyo mtu kichwani. Hivyo kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu.
19 Kuhani atatolea sadaka ya kuondoa dhambi na kumfanyia huyo mtu anayetakaswa ibada ya upatanisho ili kumwondolea unajisi wake. Kisha atamchinja mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa.
20 Kuhani atatolea ile sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya nafaka juu ya madhabahu. Hivyo kuhani atamfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho, naye atakuwa safi.
21 “Lakini ikiwa mtu huyo ni maskini, hana uwezo wa kutoa vitu hivyo, basi ataleta mwanakondoo dume mmoja kuwa fidia ya sadaka ya kuondoa hatia ambaye atafanyiwa ishara ya kutoa sadaka ili kumfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho. Ataleta pia kilo moja ya unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka na mafuta theluthi moja ya lita.