8 Huyo mtu atayafua mavazi yake, atanyoa nywele zake, na kuoga; naye atakuwa safi. Baada ya hayo atarudi kambini, lakini atakaa nje ya hema lake kwa muda wa siku saba.
9 Siku ya saba atanyoa nywele zake zote, ndevu na kope za macho yake. Kisha atafua mavazi yake na kuoga, ataoga kwa maji; naye atakuwa safi.
10 “Siku ya nane ataleta wanakondoo madume wawili wasio na dosari, kondoo jike wa mwaka mmoja asiye na dosari, kilo tatu za unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka pamoja na mafuta theluthi moja ya lita.
11 Kuhani atakayemtakasa mtu huyo atamleta mbele ya Mwenyezi-Mungu karibu na mlango wa hema la mkutano pamoja na vitu alivyoleta.
12 Kuhani atachukua mwanakondoo dume mmoja na kumtolea sadaka ya kuondoa hatia pamoja na yale mafuta theluthi moja ya lita. Atafanya ishara ya kuvitolea mbele ya Mwenyezi-Mungu.
13 Kisha atamchinja huyo mwanakondoo katika mahali patakatifu, wanapochinjia wanyama wa sadaka ya kuondoa dhambi na sadaka ya kuteketezwa. Sadaka hii ya kuondoa hatia, kama ilivyo sadaka ya kuondoa dhambi, ni mali yake kuhani; ni sadaka takatifu kabisa.
14 Kuhani atachukua kiasi cha damu ya sadaka ya kuondoa hatia na kumpaka mtu anayetakaswa katika ncha ya sikio lake la kulia na kidole gumba cha mkono wake wa kulia na kidole gumba cha mguu wake wa kulia.