1 Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose huko mlimani Sinai,
2 “Waambie Waisraeli hivi: Mtakapofika katika nchi ninayowapeni mimi Mwenyezi-Mungu kila mwaka wa saba nchi itapumzishwa isilimwe kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu.
3 Kwa muda wa miaka sita mtailima nchi, mtapanda, mtapogoa mizabibu yenu na kuvuna mazao yenu.
4 Lakini mwaka wa saba utakuwa ni sabato ya mapumziko rasmi; ni sabato ya Mwenyezi-Mungu. Msipande chochote wala kuipogoa mizabibu yenu.
5 Chochote kinachoota peke yake msikivune wala kuchuma zabibu kutoka miti isiyopogolewa. Huo utakuwa mwaka wa kuipumzisha ardhi rasmi.
6 Hata hivyo mwaka huo wa pumziko rasmi kwa nchi utawapa chakula nyinyi wenyewe, watumwa wenu wa kiume na wa kike, watu mliowaajiri na wageni wanaokaa miongoni mwenu.