31 Mafuta yote ya mbuzi huyo atayaondoa kama aondoavyo mafuta ya wanyama wa sadaka za amani, naye kuhani atayateketeza madhabahuni, na harufu yake nzuri itampendeza Mwenyezi-Mungu. Basi, kuhani atamfanyia huyo mtu hiyo ibada ya upatanisho, naye atasamehewa.
32 “Ikiwa mtu huyo ataleta mwanakondoo kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi, basi, ataleta mwanakondoo jike asiye na dosari.
33 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mwanakondoo huyo wa sadaka ya kuondoa dhambi, na kumchinjia mahali pale wanapochinjia wanyama wa sadaka za kuteketezwa.
34 Kisha kuhani atachovya kidole chake katika damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuzipaka pembe za madhabahu ya kuteketezea sadaka. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu.
35 Kisha atayaondoa mafuta yote kama aondoavyo mafuta ya mwanakondoo wa sadaka ya amani, na kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, pamoja na sadaka zitolewazo kwa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Naye kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa.”