5 Ndipo viongozi wa Yuda watakapoambiana, ‘Wakazi wa Yerusalemu wamepata nguvu yao kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wao’.
6 “Siku hiyo, viongozi wa Yuda nitawafanya kama chungu cha moto mkali katika msitu; naam, kama mwenge uwakao kati ya miganda. Watayateketeza mataifa yote yaliyo kandokando yao. Lakini watu wa Yerusalemu wataendelea kuishi salama katika mji wao.
7 “Nami Mwenyezi-Mungu nitawasaidia kwanza jamaa za Yuda kusudi wazawa wa Daudi na wakazi wa Yerusalemu wasijione kuwa maarufu zaidi ya watu wengine wa kabila la Yuda.
8 Siku hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nitawalinda wakazi wa mji wa Yerusalemu; walio wanyonge zaidi miongoni mwao watakuwa na nguvu kama mfalme Daudi. Wazawa wa Daudi watashika usukani kuwaongoza watu wa Yuda kama malaika wangu mimi Mwenyezi-Mungu, naam, kama mimi Mungu mwenyewe.
9 “Siku hiyo, nitayaangamiza mataifa yote yanayotaka kuushambulia mji wa Yerusalemu.
10 Wazawa wa Daudi na wakazi wa mji wa Yerusalemu nitawajaza roho ya huruma na maombi, nao watamtazama yeye waliyemtoboa; watamlilia kama mtu amliliavyo mtoto wake wa pekee, au kama mtu amliliavyo kwa uchungu mzaliwa wake wa kwanza.
11 Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu mjini Yerusalemu kama maombolezo ya kumwombolezea Hadad-rimoni katika mbuga za Megido.