22 Akamwambia yule aliyekuwa juu ya hazina ya mavazi, Uwatolee mavazi wote wanaomwabudu Baali. Akawatolea mavazi.
23 Akaingia Yehu na Yehonadabu mwana wa Rekabu nyumbani mwa Baali, akawaambia waliomwabudu Baali, Tafuteni mkaangalie, asiwepo hapa pamoja nanyi mtu amtumikiaye BWANA, ila wamwabuduo Baali peke yao.
24 Wakaingia ili watoe dhabihu na sadaka za kuteketezwa. Basi Yehu alikuwa amejiwekea nje watu themanini, akasema, Mtu mmoja akiokoka wa watu niliowatia mikononi mwenu, amwachaye huyo, roho yake itakuwa badala ya roho yake.
25 Ikawa mara alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa, Yehu akawaambia walinzi na maakida, Ingieni mwapige; mtu awaye yote asitoke. Basi wakawapiga kwa makali ya upanga; walinzi na maakida wakawatupa nje, wakaenda mpaka mji wa nyumba ya Baali.
26 Wakazitoa nguzo zilizokuwamo nyumbani mwa Baali, wakaziteketeza.
27 Wakaibomoa nguzo ya Baali, na kuiangusha nyumba ya Baali, wakaifanya choo hata leo.
28 Ndivyo Yehu alivyomharibu Baali katika Israeli.