1 Katika mwaka wa kumi na saba wa Peka mwana wa Remalia Ahazi mwana wa Yothamu mfalme wa Yuda alianza kutawala.
2 Alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita katika Yerusalemu; wala hakufanya mema machoni pa BWANA Mungu wake, kama Daudi babaye.
3 Lakini aliiendea njia ya wafalme wa Israeli, hata akampitisha mwanawe motoni, sawasawa na machukizo ya mataifa BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.
4 Kisha akatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti mbichi.
5 Hapo ndipo akakwea Resini mfalme wa Shamu pamoja na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli juu ya Yerusalemu ili wapigane; wakamhusuru Ahazi, ila hawakuweza kumshinda.
6 Wakati huo Resini mfalme wa Shamu akawarudishia Washami Elathi, akawafukuza Wayahudi kutoka Elathi; nao Washami wakaja Elathi, wakakaa humo hata leo.
7 Basi Ahazi akatuma wajumbe kwa Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akasema, Mimi ni mtumishi, tena mwana wako; kwea, ukaniokoe mkononi mwa mfalme wa Shamu, na mkononi mwa mfalme wa Israeli, walioniinukia.