12 wakatumikia sanamu, ambazo BWANA aliwakataza, akasema, Msitende jambo hili.
13 Pamoja na hayo BWANA aliwashuhudia Israeli, na Yuda, kwa kinywa cha kila nabii, na cha kila mwonaji, akisema, Geukeni, na kuziacha njia zenu mbaya, mkazishike amri zangu na hukumu zangu, sawasawa na ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, nikawapelekea kwa kinywa cha manabii watumishi wangu.
14 Walakini hawakutaka kusikia, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, kama shingo za baba zao, wasiomwamini BWANA, Mungu wao.
15 Wakazikataa sheria zake, na agano lake, alilolifanya na baba zao; na shuhuda zake alizowashuhudia; wakafuata ubatili, wakawa ubatili, nao wakaandamana na mataifa waliowazunguka, ambao BWANA alikuwa amewaagiza, wasitende kwa mfano wao.
16 Wakaziacha amri zote za BWANA, Mungu wao, wakajifanyizia sanamu za kusubu, yaani, ndama mbili, wakafanya na Ashera, wakaliabudu jeshi lote la mbinguni, wakamtumikia Baali.
17 Wakawapitisha watoto wao, waume na wake, motoni, wakapiga ramli, wakafanya uchawi, wakajiuza nafsi zao wapate kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, hata kumkasirisha.
18 Kwa hiyo BWANA akawaghadhibikia Israeli sana, akawahamisha mbali na uso wake; wala hapana aliyesalia ila kabila ya Yuda peke yake.