20 Basi BWANA akakikataa kizazi chote cha Israeli, akawatesa, na kuwatia katika mikono ya watu wenye kuwateka nyara, hata alipokwisha kuwatupa, watoke machoni pake.
21 Maana aliwatenga mbali Israeli na nyumba ya Daudi; nao wakamfanya Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme; Yeroboamu akawavuta Israeli wasimfuate BWANA, akawakosesha kosa kubwa.
22 Nao wana wa Israeli wakaendelea katika dhambi zote za Yeroboamu alizozifanya; hawakujiepusha nazo;
23 hata BWANA akawaondoa Waisraeli wasiwe mbele zake, kama vile alivyosema kwa kinywa cha watumishi wake wote, manabii. Basi Waisraeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe, waende nchi ya Ashuru, hata leo.
24 Naye mfalme wa Ashuru akaleta watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya Samaria badala ya wana wa Israeli; wakaumiliki Samaria, wakakaa katika miji yake.
25 Basi ikawa, wakati ule walipoanza kukaa huko, hawakumcha BWANA; kwa hiyo BWANA akapeleka simba kati yao, nao wakawaua baadhi yao.
26 Kwa hiyo wakamwambia mfalme wa Ashuru, wakasema, Wale wa mataifa uliowahamisha, na kuwaweka katika miji ya Samaria, hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi; kwa hiyo amepeleka simba kati yao, na tazama, wanawaua, kwa sababu hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi.