10 Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru.
11 Tazama, umesikia ni mambo gani wafalme wa Ashuru waliyozitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa; je! Utaokoka wewe?
12 Je! Miungu ya mataifa wale, ambao baba zangu waliwaangamiza, imewaokoa? Yaani, Gozani, na Harani, na Resefu, na wana wa Adini waliokuwa katika Telasari?
13 Yuko wapi mfalme wa Hamathi, na mfalme wa Arpadi, na mfalme wa mji wa Sefarvaimu, na wa Hena, na wa Iva?
14 Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya BWANA, akaukunjua mbele za BWANA.
15 Naye Hezekia akaomba mbele za BWANA, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia; wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi.
16 Tega sikio lako, Ee BWANA, usikie; fumbua macho yako, Ee BWANA, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, ambayo amemtuma mtu aje nayo ili kumtukana Mungu aliye hai.