3 Elisha akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha, Basi wakashuka mpaka Betheli. Basi wana wa manabii, waliokuwako Betheli, wakatoka kuonana na Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa BWANA atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akasema, Naam, najua; nyamazeni.
4 Eliya akamwambia, Tafadhali, kaa hapa, Elisha; maana BWANA amenituma niende mpaka Yeriko. Akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Nao wakafika Yeriko.
5 Basi wana wa manabii, waliokuwako Yeriko, wakamkaribia Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa BWANA atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akajibu, Naam, najua, nyamazeni.
6 Eliya akamwambia, Tafadhali kaa hapa; maana BWANA amenituma niende mpaka Yordani. Akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Wakaendelea mbele wote wawili.
7 Basi watu hamsini wa wale wana wa manabii wakaenda wakasimama, kuwakabili kwa mbali; na hao wawili wakasimama karibu na Yordani.
8 Eliya akalitwaa vazi lake la juu, akalikunja, akayapiga maji, yakagawanyika huku na huku, na hao wawili wakavuka pakavu.
9 Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu.