12 kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Angalia, naleta mabaya juu ya Yerusalemu na juu ya Yuda, hata kila mtu asikiaye, masikio yake yatawasha yote mawili.
13 Nami nitanyosha juu ya Yerusalemu kamba ya Samaria, na timazi ya nyumba ya Ahabu; nami nitaifuta Yerusalemu, kama mtu afutavyo sahani, kuifuta na kuifudikiza.
14 Nami nitawatupa mabaki ya urithi wangu, na kuwatia mikononi mwa adui zao; nao watakuwa nyara na mateka kwa adui zao wote;
15 kwa sababu wametenda yaliyo mabaya machoni pangu, na kunikasirisha, tangu siku ile walipotoka baba zao katika Misri, hata leo hivi.
16 Na Manase akazimwaga damu zisizo na hatia, nyingi sana, hata alipokuwa ameijaza Yerusalemu tangu upande huu hata upande huu; zaidi ya kosa lake alilowakosesha Yuda, kutenda yaliyo mabaya machoni pa BWANA.
17 Basi mambo yote ya Manase yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na kosa lake alilolikosa, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
18 Manase akalala na babaze, akazikwa katika bustani ya nyumba yake mwenyewe, yaani, bustani ya Uza. Na Amoni mwanawe akatawala mahali pake.