3 Ikawa, katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia, mfalme akamtuma Shafani, mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, mwandishi, nyumbani kwa Bwana, akisema,
4 Enenda kwa Hilkia, kuhani mkuu, ili aihesabu fedha yote inayoletwa nyumbani mwa BWANA, ambayo mabawabu wameipokea kwa watu;
5 tena waitie ile fedha katika mikono ya wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya BWANA; wakapewe wafanya kazi waliomo ndani ya nyumba ya BWANA, ili wapate kupatengeneza mahali palipobomoka ndani ya nyumba;
6 wapewe maseremala, na wajenzi, na waashi; ili kununua miti na mawe yaliyochongwa wapate kuitengeneza nyumba.
7 Lakini hawakuulizwa habari za ile fedha waliyokabidhiwa; maana walitenda kazi kwa uaminifu.
8 Naye Hilkia, kuhani mkuu, akamwambia Shafani, mwandishi, Nimekiona kitabu cha torati katika nyumba ya BWANA. Hilkia akampa Shafani kile kitabu, naye akakisoma.
9 Shafani mwandishi akamwendea mfalme, akamletea mfalme habari tena, akasema, Watumishi wako wamezitoa zile fedha zilizoonekana ndani ya nyumba, nao wamewakabidhi wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya BWANA.