31 Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Hamutali binti Yeremia wa Libna.
32 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na yote waliyoyafanya baba zake.
33 Naye Farao-neko akamfunga huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, ili asitawale huko Yerusalemu. Akaitoza nchi kodi talanta mia za fedha na talanta ya dhahabu.
34 Farao-neko akamfanya Eliakimu mwana wa Yosia awe mfalme mahali pa Yosia babaye, akambadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu, lakini akamwondoa Yehoahazi; akaenda naye Misri, naye akafa huko.
35 Na Yehoyakimu akampa Farao dhahabu na fedha; lakini akaitoza nchi kodi, ili apate kutoa zile fedha kwa amri yake Farao; akawatoza fedha na dhahabu watu wa nchi, kila mtu kwa kodi yake, ili ampe Farao-neko.
36 Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Zebida binti Pedaya wa Ruma.
37 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na yote waliyoyafanya baba zake.