8 Yekonia alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani wa Yerusalemu.
9 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, mfano wa yote aliyoyafanya baba yake.
10 Wakati ule watumishi wa Nebukadreza mfalme wa Babeli wakakwea kwenda Yerusalemu, na mji ukahusuriwa.
11 Na Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akaufikilia huo mji, hapo watumishi wake walipokuwa wakiuhusuru.
12 Na Yekonia, mfalme wa Yuda, akatoka akamwendea mfalme wa Babeli, yeye na mama yake, na watumishi wake, na wakuu wa watu wake, na maakida wake; mfalme wa Babeli akamchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake.
13 Akatoa huko hazina zote za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme, akavikata-kata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Sulemani, mfalme wa Israeli, alivifanya katika hekalu la BWANA, kama BWANA alivyosema.
14 Akawachukua mateka watu wa Yerusalemu wote pia, na wakuu wote, na mashujaa wote, watu elfu kumi; na mafundi wote, na wafua chuma wote; hapana mtu aliyebaki, ila waliokuwa wanyonge wa watu wa nchi.