21 Naye mfalme wa Babeli akawapiga, na kuwaua huko Ribla katika nchi ya Hamathi. Hivyo Yuda wakachukuliwa utumwani kutoka nchi yao.
22 Na kwa habari ya watu waliosalia katika nchi ya Yuda, aliowasaza Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akamweka Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani awe liwali juu yao.
23 Kisha, wakuu wote wa majeshi, wao na watu wao, waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemweka Gedalia kuwa liwali, wakamwendea Gedalia huko Mispa; nao ni hawa, Ishmaeli mwana wa Nethania, na Yohana mwana wa Karea, na Seraya mwana wa Tanhumethi Mnetofa, na Yezania mwana wa Mmaaka, wao na watu wao.
24 Na Gedalia akawaapia wao na watu wao, akawaambia, Msiogope kwa ajili ya watumishi wa Wakaldayo; kaeni katika nchi; mkamtumikie mfalme wa Babeli; itakuwa vyema kwenu.
25 Lakini ikawa katika mwezi wa saba Ishmaeli mwana wa Nethania, mwana wa Elishama, mmoja wa wazao wa kifalme, na watu kumi pamoja naye, wakamwendea Gedalia, wakampiga hata akafa, na hao Wayahudi na Wakaldayo waliokuwa pamoja naye huko Mispa.
26 Wakaondoka watu wote, wadogo kwa wakubwa, pamoja na wakuu wa majeshi, wakainuka kwenda Misri; kwa kuwa waliwaogopa Wakaldayo.
27 Ikawa katika mwaka wa thelathini na saba wa kuhamishwa kwake Yekonia, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa kumi na mbili, siku ya ishirini na saba ya mwezi, Evil-merodaki, mfalme wa Babeli, katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake, akamwinua kichwa Yekonia, mfalme wa Yuda, akamtoa gerezani.