26 Tafadhali piga mbio sasa kwenda kumlaki, ukamwambie, Hujambo? Mume wako hajambo? Mtoto hajambo? Akajibu, Hawajambo.
27 Naye alipofika kwa yule mtu wa Mungu kilimani, alimshika miguu. Gehazi akakaribia amwondoe; lakini mtu wa Mungu akamwambia, Mwache; maana roho yake ndani yake ina uchungu; na BWANA amenificha, wala hakuniambia.
28 Yule mwanamke akasema, Je! Naliomba mwana kwa bwana wangu? Mimi sikusema, Usinidanganye?
29 Ndipo Elisha akamwambia Gehazi, Jikaze viuno, ukachukue fimbo yangu mkononi mwako, ukaende zako; ukikutana na mtu, usimsalimu; na mtu akikusalimu, usimjibu; ukaweke fimbo yangu juu ya uso wa mtoto.
30 Na mama yake yule mtoto akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Basi akaondoka, akamfuata.
31 Na Gehazi akawatangulia, akaiweka ile fimbo juu ya uso wa mtoto; lakini hapakuwa na sauti, wala majibu. Basi akarudi ili kumlaki, akamwambia, akisema, Mtoto hakuamka.
32 Basi Elisha alipofika nyumbani, tazama, mtoto amekwisha kufa, amelazwa kitandani pake.