28 Yule mwanamke akasema, Je! Naliomba mwana kwa bwana wangu? Mimi sikusema, Usinidanganye?
29 Ndipo Elisha akamwambia Gehazi, Jikaze viuno, ukachukue fimbo yangu mkononi mwako, ukaende zako; ukikutana na mtu, usimsalimu; na mtu akikusalimu, usimjibu; ukaweke fimbo yangu juu ya uso wa mtoto.
30 Na mama yake yule mtoto akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Basi akaondoka, akamfuata.
31 Na Gehazi akawatangulia, akaiweka ile fimbo juu ya uso wa mtoto; lakini hapakuwa na sauti, wala majibu. Basi akarudi ili kumlaki, akamwambia, akisema, Mtoto hakuamka.
32 Basi Elisha alipofika nyumbani, tazama, mtoto amekwisha kufa, amelazwa kitandani pake.
33 Basi akaingia ndani, akajifungia mlango, yeye na yule mtoto wote wawili, akamwomba BWANA.
34 Akapanda juu ya kitanda, akajilaza juu ya mtoto, akaweka kinywa chake juu ya kinywa chake, na macho yake juu ya macho yake, na mikono yake juu ya mikono yake; akajinyosha juu yake; mwili wake yule mtoto ukaanza kupata moto.